Mgomo wa kuketi wa wajumbe waandamizi wa chama cha Kongresi cha India kulalamikia sheria mpya ya uraia

Shakhsia kadhaa, wakiwemo viongozi na wajumbe waandamizi wa chama kikuu cha upinzani nchini India cha Kongresi ya Taifa (INC) wamekusanyika kwenye mnara wa kumbukumbu ya baba wa taifa hilo Mahatma Ghandhi na kufanya mgomo wa kuketi kulalamikia sheria mpya ya uraia iliyopitishwa na serikali ya nchi hiyo.

Wakati maandamano ya upinzani ya kulalamikia sheria mpya ya uraia ya India yakiwa yanaendelea katika majimbo mbali mbali ya nchi hiyo, viongozi mashuhuri wa Chama cha Kongresi ya Taifa, akiwemo waziri mkuu wa zamani Manmohan Singh, kiongozi aliyepita wa chama hicho Rahul Ghandhi, Katibu Mkuu wa chama Priyanka Ghandhi, kiongozi wa upinzani katika Baraza la Seneti Ghulam Nabi Azad na Kamal Nath, Waziri Kiongozi wa jimbo la Madhya Pradesh, wamefanya mgomo wa kuketi, mahali ulipo mnara wa kumbukumbu ya Mahatma Ghandhi katika mji mkuu wa nchi hiyo New Delhi.

Katibu Mkuu wa INC, Priyanka Ghandhi

Wafanyamgomo huo wa kuketi wanasema, sheria mpya ya uraia inapingana na katiba ya India; hivyo wametaka ifutwe. Akizungumzia suala hilo Rahul Ghandhi amesema, serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi imeleta mpasuko katika jamii ya India kwa kupitisha sheria hiyo mpya ya uraia.

Malalamiko na mgomo wa kuketi uliofanywa na wajumbe wa chama kikuu cha upinzani nchini India kupinga sheria mpya ya uraia vimedhihirisha wazi ukubwa wa malalamiko dhidi ya sheria hiyo. Tangu bunge lilipopitisha sheria hiyo, barabara za miji isiyopungua 56 katika majimbo 24 ya India imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya umma na nadra kuwahi kushuhudiwa, dhidi ya siasa na sera za kuwapiga vita Waislamu zinazotekelezwa na serikali ya Narendra Modi.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi

Wengi wanaamini kuwa maandamano ya upinzani yaliyoshuhudiwa nchini India katika wiki mbili za karibuni, ni changamoto kubwa zaidi kuwahi kukikabili chama tawala cha  Bharatiya Janata (BJP) tangu kiliposhika hatamu za madaraka mwaka 2014. Ukubwa wa maandamano yenyewe kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kutohusisha chama au mrengo fulani tu, kunaonyesha ni kwa kiwango gani hatua iliyochukuliwa na chama cha BJP imeitia wasiwasi mkubwa jamii ya nchi hiyo.

Nilanjana Roy, mwandishi wa gazeti la Financial Times linalochapishwa London, Uingereza ameandika yafuatayo katika makala yake iliyochapishwa na gazeti hilo:

“Ukandamizwaji huu wa Waislamu nchini India haujawahi kushuhudiwa; na inatabiriwa kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kutokana na ukandamizaji utakaofanywa na Polisi kuzima maandamano ya upinzani. Kutekeleza sheria kama hii kunafungua njia ya kufanya ubaguzi mkubwa zaidi dhidi ya Waislamu, ambao tayari wanaandamwa na mashinikizo ya Wahindu waliowengi.”

Taswira hiyo iliyogubikwa na wingu zito la mustakabali tata wa hali ya Waislamu nchini India ni moja ya sababu zilizoyafanya maandamano ya upinzani yawe na wigo mpana mno kiasi cha kukishtukiza na kukishangaza chama tawala cha BJP. Wakati huohuo hatua kali zinazochukuliwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji katika miji kadhaa, na ukandamizaji wa kikatili vinaowafanyia watu wanaoandamana kwa amani vimeonyesha kuwa, chama tawala kimedhamiria kuitelekeza sheria hiyo ya kibaguzi kwa gharama yoyote ile. Hii ni pamoja na dhana kiliyonayo chama hicho kwamba, maandamano hayo ya upinzani yameandaliwa na kuongozwa na wapinzani wa serikali ya chama hicho cha BJP.

Lakini pamoja na dhana hiyo kiliyonayo chama tawala, utendaji wa serikali ya Nrendra Modi, hasa baada ya kushinda tena uchaguzi wa bunge unaonyesha kuwa, serikali yake imeamua kuiandama jamii ya Waislamu wa India kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa; na hatua inazochukua zinalenga kuwapa Wahindu hadhi ya juu zaidi ya uraia; hata hivyo waliowengi wanatoa indhari juu ya matokeo mabaya ya siasa hizo za Modi.

Nilanjana Roy amelizungumzia suala hilo kama ifuatavyo katika sehemu nyingine ya makala yake:

“Watu wote inawapasa wafahamu kuwa, hakuna yeyote awezaye kuifuta jamii ya Waislamu milioni 200 katika nchi hii. Inapasa tuseme kwamba, wiki iliyopita watu walieleza wayatakayo, na idadi kubwa ya wanachuo na raia wa kawaida wamemiminika barabarani katika miji kadha wa kadha kulalamikia sheria mpya ya uraia; na yumkini hali ikawa mbaya zaidi katika siku zijazo.” 

Onyo na indhari hii ilishatolewa na watu wengi ndani ya India tangu miezi kadhaa nyuma, lakini hatua kadhaa zilizochukuliwa na chama cha BJP dhidi ya Waislamu na hatimaye kupitishwa mswada wa sheria ya uraia wa India vimeonyesha kuwa, chama hicho na serikali yake hazijali wala hazibali kusikiliza lawama na ukosoaji dhidi yake. Kwa muktadha huo, tunaweza kuuelezea mgomo wa kuketi wa wajumbe waandamizi wa chama kikuu cha upinzani cha Kongresi ya Taifa kuwa ni ishara nyingine ya kupanuka wigo wa upinzani kwa hatua zinazochukuliwa na serikali ya sasa ya India dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Hata hivyo kwa mtazamo wa chama cha Kongresi, hatua hizo si za kuwapiga vita Waislamu pekee, lakini zinailenga pia India nzima, katiba yake na vilevile misingi mikuu iliyowekwa na viongozi wa taifa hilo.